Wanaotaka nafasi ya Infantino mwisho Novemba 18

ZURICH: WAKATI Infantino anajiandaa kugombea tena nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi mwaka 2027 wagombea wengine wanaotaka kushindana naye wanapaswa kujitangaza kabla ya Novemba 18.
Hadi sasa, UEFA haijafanikiwa kupata mgombea ambaye ameonesha wazi kuwa na uungwaji mkono unaohitajika kumpa changamoto Infantino.
Hata hivyo, Rais huyo alipata msukumo muhimu Oktoba 23 baada ya Shirikisho la Soka Asia (AFC) kutangaza kumuunga mkono katika uchaguzi ujao.
Mkuu wa CONCACAF, Victor Montagliani, alikuwa ametajwa kuwa mmoja wa watu wanaoweza kugombea, lakini ametangaza nia ya kutafuta muhula mwingine katika uongozi wa shirikisho la Amerika Kaskazini, hali inayopunguza uwezekano wa kugombea urais wa FIFA.
Aliyekuwa beki wa Tottenham Hotspur, Celtic na timu ya taifa ya Uswisi, Ramon Vega, naye ametangaza utayari wa kuwania nafasi hiyo, ingawa bado haijajulikana kama atapata uungwaji mkono wa kutosha.




