Raphinha hakosei! Yamal avunja rekodi ya mbappe

BARCELONA: MSHAMBULIAJI Raphinha alifunga mabao mawili na kuiongoza Barcelona kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Aston Villa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa Jumanne usiku kwenye Uwanja wa Camp Nou.
Ushindi huo ulihitimisha mwanzo mzuri wa Aston Villa katika mashindano hayo, huku Barcelona ikirejea kwenye ushindani wa nafasi nane za juu katika hatua ya ligi baada ya kupoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Paris Saint-Germain.
Barcelona ilianza kwa kasi na kupata bao la kwanza dakika ya saba kupitia nyota wake chipukizi Lamine Yamal, aliyenufaika na kosa la Joao Gomes aliyepoteza mpira katika eneo la hatari. Yamal aliutumia vizuri mpira huo na kumshinda kipa wa Aston Villa, Zion Suzuki.
Bao hilo lilikuwa la 14 kwa Yamal katika historia yake ya kushiriki Ligi ya Mabingwa akiwa kijana, na kumwezesha kuvunja rekodi ya Kylian Mbappe aliyekuwa na mabao 13 kabla ya kufikisha umri wa miaka 20 katika mashindano hayo.
Licha ya kuruhusu bao la mapema, Aston Villa chini ya kocha Unai Emery ilijibu kwa mashambulizi kadhaa na kuonesha ushindani katika kipindi cha kwanza.
Matty Cash alikaribia kusawazisha baada ya shuti lake kali kuelekezwa langoni, lakini mpira ulizuiliwa na kwenda nje kidogo. Barcelona iliendelea kutumia presha ya juu kuisumbua Villa katika kuanzisha mashambulizi, huku kipa wake akilazimika kufanya kazi ya ziada kuzuia baadhi ya mashuti ya wapinzani. Hata hivyo, wenyeji waliendelea kuwa na uwezo mkubwa wa kutumia nafasi muhimu walizozipata.
Kipindi cha pili kilianza kwa Barcelona kuongeza nguvu katika mashambulizi na kupata bao la pili kupitia Raphinha aliyepokea pasi ya Fermin Lopez kabla ya kuonesha ustadi wa miguu na kuuweka mpira wavuni dakika za mwanzo za kipindi hicho. Mshambuliaji huyo wa Brazil alikamilisha mabao yake mawili baada ya kupokea krosi nzuri ya Joao Cancelo iliyopigwa kwa nje ya mguu, na kufunga karibu na lango na kuifanya Barcelona kuongoza kwa mabao 3-0. Bao hilo lilikuwa la 19 kwa Raphinha katika mashindano yote msimu huu, likiimarisha mchango wake katika safu ya ushambuliaji ya miamba hiyo ya Hispania.
Baada ya mchezo huo, Raphinha alieleza furaha yake kwa ushindi huo lakini akasema hakutaka kuzungumzia zaidi soka kutokana na kifo cha mshambuliaji Jesus De Miguel wa Tenerife, aliyefariki Jumanne asubuhi kufuatia kugongana na mchezaji mwenzake wakati wa mchezo wa ligi daraja la pili nchini Hispania.
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, amepongeza nidhamu ya kikosi chake katika ulinzi, akisema wachezaji walicheza kwa mshikamano na kuhakikisha Aston Villa haipati nafasi nyingi za kufunga. Ushindi huo pia umeiwezesha Barcelona kupata clean sheet yake ya kwanza katika michezo 19 ya Ligi ya Mabingwa. Kwa upande wake, nahodha wa Aston Villa, John McGinn, amesema mchezo huo umekuwa somo muhimu kwa timu yake, huku Unai Emery akikiri kuwa Barcelona ilitumia vizuri nafasi zake na kusisitiza umuhimu wa kikosi chake kuboresha umakini katika eneo la ushambuliaji.
Licha ya kipigo hicho, Aston Villa imeendelea kuwa katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa muda wa hatua ya ligi, ikiwa nafasi ya tatu.




