Dladla ataja tofauti ya Shabalala na Boka

KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga, Simo Dladla, ameweka wazi tofauti ya kiuchezaji kati ya Mohamed Hussein ‘Shabalala’ na Shadrack Boka, akisema kila mmoja ana ubora wake unaochangia mafanikio ya timu hiyo.
Dladla amesema Shabalala ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi sahihi (accuracy pass), huku akiwa na akili ya kufikiri haraka na kufanya maamuzi sahihi anapokuwa uwanjani.
Amesema tofauti na Shabalala, Boka ana kasi kubwa (speed) na uwezo wa kucheza kwa nguvu na kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake uwanjani.
Kocha huyo amesema ubora na tofauti za wachezaji hao wawili zimemfanya kutumia mfumo wa kuwabadilisha katika kikosi, ambapo mmoja anaweza kucheza mchezo mmoja na mwingine kupata nafasi katika mchezo unaofuata.
Ameeleza kuwa uamuzi huo unatokana na ukweli kwamba wote wana uwezo tofauti lakini muhimu kwa mahitaji ya timu, hivyo kuwapa nafasi kwa kupokezana kunasaidia kupata mchango wa kila mmoja.
Dladla amesisitiza kuwa lengo lake ni kutumia ubora wa wachezaji hao kwa namna itakayoiwezesha Yanga kupata matokeo mazuri na kufikia lengo kuu la timu ambalo ni ushindi.




