Maandamano Ufaransa yahairisha michezo ya Raga TOP 14

PARIS: MCHEZO wa Ligi Kuu ya Raga nchini Ufaransa (Top 14) kati ya RC Vannes na Union Bordeaux-Bègles umeahirishwa kwa siku moja na sasa utachezwa Jumapili badala ya Jumamosi kutokana na changamoto za kiusalama zinazohusishwa na maandamano yanayoendelea nchini humo.
Shirikisho la Ligi ya Raga nchini Ufaransa (LNR) limethibitisha mabadiliko hayo Alhamisi, likieleza kuwa uamuzi umefikiwa baada ya ombi kutoka kwa uongozi wa eneo husika kuhusu upatikanaji wa vikosi vya usalama.
Mchezo huo, uliokuwa umepangwa kuanza saa 13:30 GMT siku ya Jumamosi, utachezwa katika jiji la Nantes, huku ratiba ya mchezo wa Toulouse dhidi ya Clermont ikisogezwa mbele kutoka Jumapili ili kujaza nafasi iliyoachwa katika matangazo ya televisheni.
RC Vannes iliamua kuhamishia mchezo huo katika uwanja wa Stade de la Beaujoire wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 35,000, tofauti na uwanja wake wa nyumbani wa Stade de la Rabine unaochukua watu 12,500.
Hatua hiyo inakuja wakati Ufaransa ikikabiliwa na maandamano makubwa yanayohusishwa na kupanda kwa gharama za maisha. Wiki iliyopita, serikali ilipeleka maafisa 70,000 wa usalama nchini kote kusimamia maandamano hayo.
Maandamano hayo yamekuwa yakikumbwa na vurugu, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa majengo ya umma, uporaji wa maduka na kukamatwa kwa watu 2,700.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ameonya kuwa maandamano yaliyopangwa kufanyika mwishoni mwa wiki yanaweza kuleta hatari kubwa kwa usalama wa umma.
Hata hivyo, si mchezo huo pekee uliokumbwa na mabadiliko ya ratiba kutokana na hali hiyo, kwani mchezo wa Ligi Kuu ya Ufaransa kati ya Paris Saint-Germain na Lyon nao uliahirishwa kwa siku moja Jumapili iliyopita kufuatia ombi la polisi.




