Priyanka Chopra aibukia kwenye utayarishaji wa filamu

MUMBAI: MWIGIZAJI na mtayarishaji wa filamu kutoka India, Priyanka Chopra Jonas, anatarajiwa kuonekana katika filamu fupi ya ‘We Were Here’ kama mtayarishaji mtendaji na si muigizaji huku akilenga filamu hiyo kuwania tuzo za Oscar.
Filamu hiyo iliyoongozwa na Pranav Bhasin, tayari imekidhi vigezo vya kuwania tuzo za Academy Awards na imefanikiwa kutwaa zaidi ya tuzo 20 katika matamasha mbalimbali za kimataifa za filamu.
Mbali na Chopra Jonas, mradi huo pia umewashirikisha mwigizaji Andrew Scott pamoja na mwandishi wa tamthilia na mwanaharakati V, ambaye ametunukiwa tuzo ya Tony, kama mtayarishaji bora.
Akieleza sababu za kujiunga na mradi huo, Chopra Jonas amesema alivutiwa na namna filamu hiyo inavyowasilisha mada yenye umuhimu mkubwa katika dunia ya sasa, kwa kutumia mtindo wa kipekee unaochanganya ucheshi na ujumbe mzito.
Amesema ameamua kuunga mkono timu ya wabunifu wa filamu hiyo ili kusaidia kuipa nafasi kazi yao ya kipekee na kuhakikisha maono yao yanafika kwa watazamaji wengi zaidi.
Filamu ya ‘We Were Here’ inasimulia maisha ya wanaume watatu waliostaafu katika mji mdogo nchini India, ambao wanaamini mashine zinachukua nafasi za ajira za binadamu. Katika kuonesha upinzani wao, wanaamua kuandamana kwa kujifanya vifaa vya nyumbani.
Hata hivyo, maandamano yao yanachukua mwelekeo usiotarajiwa baada ya mtoto wa mmoja wao kujiunga na kampuni inayojihusisha na teknolojia ya akili mnemba (AI), hatua inayochochea mjadala kuhusu maendeleo ya teknolojia, ajira na nafasi ya binadamu katika jamii.



