Mtayarishaji wa filamu India afariki dunia

INDIA: MTAYARISHA na mkurugenzi mkongwe wa vipindi vya televisheni, Brijendra Pal Singh, maarufu kama BP Singh, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75, akiacha kumbukumbu kubwa kupitia vipindi maarufu vya upelelezi na kutisha nchini India.
Singh alifariki dunia Jumanne asubuhi, Oktoba 27, 2026, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na gazeti la Hindustan Times.
Alijulikana zaidi kwa kuanzisha na kuongoza utayarishaji wa kipindi cha upelelezi cha CID, kilichokuwa miongoni mwa vipindi vilivyodumu kwa muda mrefu katika televisheni ya India.
Mwigizaji Dayanand Shetty, aliyejipatia umaarufu kupitia nafasi ya Daya katika CID, alieleza kusikitishwa na kifo cha mtayarishaji huyo, akisema alikuwa mtu aliyejikita sana katika kazi yake na mwenye mapenzi makubwa na utengenezaji wa maudhui.
Shetty alisema Singh alikuwa na changamoto za kiafya kwa kipindi fulani kabla ya kifo chake. Aliongeza kuwa mtayarishaji huyo alikuwa pia mpiga picha wa filamu mwenye ujuzi mkubwa, aliyethaminiwa na watu aliokuwa akifanya nao kazi katika tasnia ya televisheni.
Mbali na CID, Singh alijulikana kwa kuunda kipindi cha kutisha cha Aahat, kilichokuwa maarufu kwa hadithi zake za kutisha na matukio ya kusisimua. Kipindi hicho kilimsaidia kujenga nafasi yake katika tasnia ya burudani ya India.
Kipindi cha CID kilianza kurushwa mwaka 1998 na kikapata umaarufu mkubwa kutokana na visa vya uhalifu vilivyochunguzwa na timu ya wapelelezi.
Kupitia kipindi hicho, Singh alishirikiana na waigizaji mbalimbali, akiwemo Shetty, ambaye mhusika wake wa Daya alipendwa na watazamaji wengi.
Kifo cha Singh kinaacha pengo katika tasnia ya televisheni ya India, hasa kwa mashabiki wa CID na Aahat waliovutiwa na kazi zake kwa miaka mingi. Mchango wake katika kuendeleza vipindi vya upelelezi na kutisha utaendelea kukumbukwa na watazamaji wa kazi hizo.




