Antonelli kukaribia kuweka historia Formula One

AUSTIN: DEREVA wa Mercedes, Kimi Antonelli, amesema ataendelea kuwa na mtazamo uleule anapoelekea katika mashindano ya Formula One nchini Mexico wiki ijayo, akihitaji pointi mbili pekee kutwaa ubingwa wa dunia na kuwa bingwa mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya mchezo huo.
Antonelli, raia wa Italia mwenye umri wa miaka 20, alionyesha kiwango cha juu katika mashindano ya United States Grand Prix yaliyofanyika Jumapili, Oktoba 25, akitwaa ushindi wake wa tisa msimu huu.
Ushindi huo umemuweka katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la dunia, huku akihitaji pointi mbili pekee katika mashindano yajayo nchini Mexico ili kufanikisha azma yake.
Akifanikiwa, Antonelli atavunja rekodi inayoshikiliwa na Sebastian Vettel, ambaye alitwaa ubingwa wake wa kwanza mwaka 2010 akiwa na umri wa miaka 23 na siku 133.
Dereva huyo wa Mercedes amekuwa akionyesha ushindani mkubwa msimu huu, huku ushindi wake wa Austin ukiimarisha matumaini ya timu hiyo kuona kijana huyo akiandika historia katika mashindano ya Formula One.
Hata hivyo, macho yote yataelekezwa kwenye mashindano ya Mexico wiki ijayo, ambapo Antonelli atakuwa na nafasi ya kuhakikisha ubingwa huo kwa kupata pointi anazohitaji na kutimiza ndoto ya kuwa bingwa mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Formula One.




