Kikapu

Simba, Yanga zatakiwa kuwa na timu za kikapu

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amezitaka klabu za soka nchini, ikiwemo Simba na Yanga, kuangalia uwezekano wa kuanzisha timu za mpira wa kikapu ili kupanua wigo wa uwekezaji na kuongeza ushindani katika michezo.

Akizungumza kwenye fainali ya ligi ya kikapu Dar es Salaam kati ya Dar City dhidi ya Stein Warriors Makonda amesema klabu hizo zina nafasi ya kupanua shughuli zake kwa kushiriki katika michezo mingine, akieleza kuwa majina ya Simba Sports Club na Yanga Sports Club yanaweza kwenda sambamba na umiliki wa timu za kikapu.

Amesema tayari wamewasilisha ombi kwa Waziri Mkuu kuhusu uwezekano wa klabu za soka kuwa na timu za kikapu, akiamini hatua hiyo inaweza kuongeza wadau na wawekezaji katika mchezo huo.

Kuhusu Azam, amesema wana mpango wa kuwasilisha mapendekezo kwa uongozi wa kampuni hiyo ili kuona uwezekano wa kuanzisha timu ya kikapu hatua itakayosaidia kukuza mchezo huo na kuongeza ushindani.

Katika hatua nyingine, Makonda ameishukuru Azam Media kwa mchango wake katika kukuza mchezo huo , akisema kampuni hiyo haijaishia kuonesha matangazo ya moja kwa moja na kutangaza mashindano, bali imeongeza udhamini wake mwaka huu ili kusaidia mashindano ya Taifa Cup.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Hasheem Thabit, amesema kikapu inaweza kubadilisha maisha ya vijana na familia zao, akiwahimiza wazazi kuwapa watoto nafasi ya kushiriki mchezo huo na kukuza vipaji vyao.

Thabit ameiomba Serikali kuendelea kusaidia vijana wenye vipaji kwa kuweka mazingira bora ya kuwawezesha kuendeleza uwezo wao kupitia michezo. Pia amewashukuru viongozi, mashabiki na wadhamini waliojitokeza kufanikisha hafla hiyo.

Related Articles

Back to top button