
KIGALI: BAADA ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 35, Formula 1 inatarajiwa kurejea barani Afrika mwaka 2030, huku Rwanda ikitajwa kuwa mwenyeji wa mbio hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya RacingNews365, makubaliano tayari yamefikiwa, huku tangazo rasmi likitarajiwa kutolewa kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Iwapo mpango huo utathibitishwa, utakuwa mwanzo wa sura mpya kwa Formula 1 barani Afrika, ambalo limekuwa nje ya kalenda ya mashindano hayo tangu 1993, wakati Grand Prix ya Afrika Kusini ilipofanyika.
Rwanda ilianza rasmi kuonesha nia ya kuwa mwenyeji wa Formula 1 mwaka 2024, baada ya Rais Paul Kagame kutangaza mpango wa nchi hiyo kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo, changamoto kubwa ilikuwa kutokuwepo kwa uwanja wa kisasa wa mbio wenye uwezo wa kuandaa mashindano ya kiwango cha Formula 1.
Sasa, mipango inaendelea kujenga uwanja mpya wa kudumu wa mbio nje kidogo ya Kigali, ambao unatarajiwa kukidhi viwango vinavyohitajika kwa mashindano hayo makubwa ya magari.
Formula 1 imekuwa ikitafuta fursa ya kurejea Afrika, huku juhudi mbalimbali zikifanyika ili bara hilo lirudi kwenye kalenda ya mashindano.
Kwa Rwanda, kuwa mwenyeji wa Formula 1 kutakuwa tukio kubwa la kimataifa na hatua muhimu katika jitihada zake za kujenga hadhi kama kitovu cha michezo na matukio makubwa barani Afrika.
Ikiwa makubaliano hayo yatathibitishwa, mwaka 2030 unaweza kuwa mwanzo wa safari mpya ya Formula 1 barani Afrika, safari itakayorejesha magari yenye kasi kubwa zaidi duniani kwenye ardhi ya bara hilo baada ya zaidi ya miongo mitatu.




