Michezo Mingine

Vodacom Coastal Classic yaunganisha michezo, utalii Afrika

PWANI: Uzinduzi wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic 2026 umeonesha namna michezo inavyoweza kuwa chachu ya kukuza utalii, elimu na maendeleo ya jamii nchini Tanzania.

Mashindano hayo ya baiskeli yametoa fursa ya kuonesha vivutio vya utalii vilivyopo katika ukanda wa pwani, huku yakiunga mkono shughuli zenye manufaa ya muda mrefu kwa jamii zitakazopitiwa na msafara wa Nyerere Cycling Tour, kutoka Dar es Salaam hadi Butiama.

Waendesha baiskeli 147 walishiriki mashindano hayo yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya kuvutia ya ukanda wa pwani. Mbali na ushindani, mashindano hayo yamelenga kukuza utalii wa ndani, kuhamasisha vijana kupitia michezo na kuongeza uelewa kuhusu elimu, afya na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Mwandamizi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Charles Maguzu, aliwapongeza waandaaji na washiriki kwa kutumia michezo kama jukwaa la kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Vodacom Coastal Classic ni ushahidi wa namna mchezo wa baiskeli unavyozidi kuwa na nafasi muhimu katika kuhamasisha maisha yenye afya, kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji na kuonesha vivutio vya utalii vya Tanzania,” alisema.

Washindani wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic wakiwa katika eneo la kuanzia mashindano hayo kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kuelekea Bagamoyo, wakimsikiliza Mkurugenzi wa Tehama wa Vodacom Tanzania Plc Athumani Mlinga

Katika mashindano hayo, Charles Kagimu na Mary Aleper, wote kutoka Uganda, waliibuka washindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake. Kila mmoja alizawadiwa Sh milioni 10.

Washindi wa nafasi ya pili walipata Sh milioni 7, huku waliomaliza nafasi ya tatu wakipata Sh milioni 5. Waliomaliza nafasi ya nne hadi ya 10 katika kila kundi walizawadiwa Sh milioni 1 kila mmoja.

Mkurugenzi wa Vodacom Business kutoka Vodacom Tanzania PLC Nguvu Kamando (kulia), na mwanzilishi wa msafara wa baiskeli wa Nyerere Cyling Tour Gabriel Landa kushoto, wakiwa kwenye picha ya pamoja na washindi wa mashindano wa Cycling Tour Upande wa wanawake, Mary Aleper kutoka Uganda aliyeshika nafasi ya kwanza (katikati), Ditona Munu Martinie kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliyeshika nafasi ya pili (wa pili kushoto), na Mercy Elegae kutoka Kenya aliyeshika nafasi ya tatu (wa pili kulia). Washindi hao walijishindia kiasi cha shilingi milioni 10, milioni saba na milioni tano kila mmoja.

Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania PLC, Nguvu Kamando, alisema mashindano hayo yataendelea kutoa fursa kwa waendesha baiskeli kuonesha vipaji vyao na kuchangia katika maendeleo ya taifa.

“Zaidi ya ushindani wenyewe, Vodacom Coastal Classic na Nyerere Cycling Tour zinasaidia kukuza utalii wa ndani, kuunga mkono shughuli za elimu na kuhamasisha matokeo chanya ya kijamii katika jamii zinazopitiwa na safari hii,” alisema.

Mshindi wa Kwanza wa Mashindano ya Vodacom Coastal Classic upande wa wanaume Charles Kagimu kutoka Uganda (katikati) mshindi wa pili Jordan Schleck kutoka Uganda (kushoto) na mshindi wa tatu Boniphace Ngwata kutoka Tanzania (kulia), wakionesha mfano wa hundi walizokabidhiwa katika mashindano hayo. Washindi hao walijishindia milioni 10 kwa mshindi wa kwanza, milioni 7 kwa mshindi wa pili, na milioni 5 kwa mshindi wa tatu mtawalia.

Kwa upande wake, Meneja wa Uendelevu wa Stanbic Bank Tanzania, Annette Nkini, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya benki hiyo katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Nyerere Cycling Tour itahusisha safari ya kilomita 1,500 kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, kuanzia Oktoba 5 hadi 14, 2026. Safari hiyo itawakutanisha waendesha baiskeli kutoka Tanzania na nchi nyingine, sambamba na shughuli za elimu, afya na uhifadhi wa mazingira katika maeneo yatakayopitiwa.

Washiriki wa Mashindano ya Nyerere Cycling Tour wakiendelea na Mashindano hayo ukanda wa Pwani wa bahari ya Hindi kuelekea Bagamoyo

Vodacom Tanzania ni mshirika mkuu wa Nyerere Cycling Tour, huku Afro Oil, Stanbic Bank Tanzania, BYD, ABC, Coca-Cola na Huawei wakiwa miongoni mwa washirika wanaounga mkono mpango huo.

Kumalizika kwa Vodacom Coastal Classic kunaweka msingi wa kuanza kwa safari ya Nyerere Cycling Tour kuelekea Butiama, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Related Articles

Back to top button