Diamond Platnumz: Rayvanny na Jux hawana cha kunifundisha kwenye imani, Joel Lwaga ananishauri

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Tanzania, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, amezungumza kuhusu suala la imani na namna marafiki zake wanavyomshauri katika maisha yake ya kila siku.
Akizungumza katika Usiku wa ‘Nikumbuke’, uliofanyika katika Superdome, Masaki, ambapo mtumishi wa Mungu, Joel Lwaga, alikuwa akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa pamoja na watu wenye mahitaji maalumu, Diamond alisoma mistari kutoka katika Biblia, kitabu cha Luka 5:31–32.
Diamond amesema anamthamini na kumpenda rafiki yake Joel Lwaga, akirejea mafundisho ya Yesu kwamba alikuja kwa ajili ya waliopotea na wenye dhambi, na si kwa ajili ya wale wanaojiona kuwa watakatifu pekee.
Katika maelezo yake, Diamond alitofautisha ushauri anaoupata kutoka kwa wasanii wenzake, akiwataja Rayvanny na Jux, na ule anaoupata kutoka kwa Joel Lwaga kuhusu masuala ya imani na matendo yanayompendeza Mungu.
Diamond amesema Rayvanny na Jux, kwa kuwa wote wako katika tasnia ya muziki, hawawezi kumpa ushauri wa kina kuhusu masuala ya imani kwa namna ambayo Joel Lwaga amekuwa akifanya.
Kwa upande wake, Diamond amesema Joel Lwaga amekuwa akimkumbusha na kumshauri mara kwa mara kuhusu umuhimu wa kufanya mambo yanayompendeza Mungu.
Kauli hiyo imeibua mjadala kuhusu urafiki, muziki na namna wasanii wanavyoweza kupeana ushauri katika masuala ya maisha na imani.
Tukio hilo la ‘Nikumbuke’ lilihudhuriwa na watu mbalimbali, huku Joel Lwaga akisherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kushirikiana na watu wenye mahitaji maalumu.




