MasumbwiMichezo Mingine

Kidunda atamba kushinda pambano

BONDIA wa uzito wa Super Middle, Selemani Kidunda amesema kuwa maandalizi ya pambano lake dhidi ya Patrick Mukala yanaendelea vizuri, anawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kumpa sapoti Februari 24 atakapokuwa akiipeperusha bendera ya nchi.

Pambano hilo la kuwania mkanda wa ubingwa wa ABU la raundi 10, limeandaliwa na Promota Saada Kasonso kutoka kampuni ya Kemmon Sports Agency.

Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Kidunda, amesema anajua kiu ya mashabiki wake ni
kuona anaibuka na ushindi katika pambano lijalo dhidi ya Mukala, ambaye hii itakuwa mara ya kwanza kukutana na bondia huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

“Lengo langu ni kukusanya mikanda tofauti ili kuongeza thamani yangu, lakini pia najua mashabiki wangu wanatamani kuona kile kilichotokea katika pambano lililopita, nawaahidi
kuwa pambano hili litakuwa la kuendeleza ubabe wangu kwenye ardhi ya nyumbani na kuipeperusha bendera ya nchi.”

Kidunda na Mukala watapanda ulingoni katika pambano hilo ikiwa ni baada ya kupita miezi sita tangu Kidunda alivyomchapa kwa pointi Tshimanga Katompa kutoka DR Congo Julai mwaka jana katika pambano la kuwania ubingwa wa dunia wa WBF kwenye pambano ambalo lilipigwa Songea mkoani Ruvuma.

Naye promota Kasonso, amesema kuwa mashabiki wa ngumi wakae mkao wa kula kwani wamepanga kuleta mapinduzi ya mchezo wa ngumi hapa nchini.

“Ukiondoa pambano hilo ambalo litakuwa ndiyo kubwa, tutakuwa na mapambano mengi ya utangulizi ambayo yatawakutanisha mabondia 18 katika mapambano tisa ambayo yote yatakuwa makali kutokana na aina ya mabondia watakaopanda ulingoni siku hiyo ingawa kwa sasa kama waandaaji tunakaribisha wadhamini ili kuweza kusapoti pambano letu,” amesema Kasonso.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button