Tom Holland nmwigizaji anayeingiza fedha nyingi zaidi

LOS ANGELES: Mwigizaji wa Uingereza, Tom Holland, mwenye umri wa miaka 30, ameweka historia mpya katika tasnia ya filamu duniani baada ya kuwa mwigizaji mwenye pato kubwa zaidi ya filamu kwa ujumla, akiwapita mastaa wakubwa akiwemo Tom Cruise, Robert Downey Jr., Scarlett Johansson na Zoe Saldana.
Holland amefikia rekodi hiyo baada ya mafanikio makubwa ya filamu mpya ya ‘Spider-Man: Brand New Day’, ambayo imeingiza takribani dola bilioni 2.45 katika mauzo ya tiketi duniani.
Kwa jumla, filamu 24 ambazo amekuwa mhusika mkuu zimekusanya zaidi ya dola bilioni 15.55 katika mapato ya kimataifa.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, Zoe Saldana anashika nafasi ya pili akiwa na takribani dola bilioni 15.47, akifuatiwa na Scarlett Johansson mwenye dola bilioni 15.40, Chris Pratt dola bilioni 15.15 na Samuel L. Jackson dola bilioni 14.6.
Orodha hiyo pia inawajumuisha nyota wengine wakubwa wa Hollywood, akiwemo Robert Downey Jr. mwenye dola bilioni 14.3,
Chris Hemsworth dola bilioni 12.19, Vin Diesel dola bilioni 12.04 na Chris Evans dola bilioni 11.49.
Tom Cruise ndiye mwigizaji pekee asiyehusishwa na Marvel katika orodha hiyo ya 10 bora, akiwa na mapato ya takribani dola bilioni 13.37 kutokana na filamu zake 45.
Safari ya Holland kuelekea kileleni ilianza akiwa mtoto, alipoanza kuigiza jukwaani akiwa na umri wa miaka 11.
Alianza katika filamu ‘The Impossible’ mwaka 2012, kabla ya kuonekana katika filamu nyingine ya ‘How I Live Now’ na ‘Locke’.
Mabadiliko makubwa katika maisha yake ya kisanii yalitokea mwaka 2015, aliposaini mkataba wa filamu sita na Marvel Studios kucheza Spider-Man.
Alionekana kwa mara ya kwanza katika ‘Captain America: Civil Wa’r, filamu iliyovuka mapato ya dola bilioni moja duniani.
Tangu wakati huo, filamu nne za Spider-Man alizoigiza Holland zimekusanya zaidi ya dola bilioni 6.3, huku pia akiongeza mapato kupitia ‘Avengers: Infinity War’ na ‘Avengers: Endgame’.
Nje ya ulimwengu wa Marvel, ameshiriki katika filamu zilizofanikiwa kama Uncharted na The Odyssey.
Mwaka 2026 umekuwa wa kipekee zaidi kwake, kwani filamu zake mbili zilizotoka mwaka huo zimekusanya zaidi ya dola bilioni 4.1. Holland pia anatarajiwa kuongeza zaidi rekodi yake kupitia filamu Avengers: Doomsday, inayotarajiwa kutoka baadaye mwaka huu.




