Binti wa Mayweather kulipa fidia ya bilioni 132

TEXAS: IYANNA ‘Yaya’ Mayweather ambaye ni binti wa bondia Floyd Mayweather ameamriwa na mahakama kumlipa Lapattra Jacobs Dola milioni 50 (sawa na Sh bilioni 132.3).
Fedha hizo ni fidia ya kumchoma visu Lapattra kwenye ugomvi baina yao uliotokea mwaka 2020 wakimgombania rapa NBA Youngboy.
Jaji wa mahakama ya Texas, alieleza kuwa Dola milioni 40 ni fidia ya gharama za matibabu, maumivu, mateso, ulemavu wa mkono, kupoteza uwezo wa kupata kipato na makovu.
Na ongezeko la Dola milioni 10 ni fidia nyingine iliyojumuishwa kama onyo na funzo kwa wengine kwa tabia hizo mbovu.
Aidha, Lapattra alifungua mashtaka hayo pia kwa mzazi mwenza, NBA lakini mahakama haikupeleka shauri hilo kizimbani.
Yaya, 26 alikamatwa mwaka 2020 nyumbani kwa NBA, 26 wakati Lapattra, 31 akiwa amelala chini baada ya kujeruhiwa mara mbili kwa kisu.
Mwaka 2022, Yaya alipandishwa kizimbani na kukiri kosa kisha kuhukumiwa kifungo cha nje kwa miaka sita chini ya uangalizi mkali kabla ya hukumu hii mpya kutoka ya kulipa fidia hizo.




