Muziki

Luizer Mbutu awasihi wanawake kutunza ngozi zao

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa dansi, Luizer Nyoni Mbutu, amewashauri mabinti na wanawake kuthamini na kutunza ngozi zao kwa kuepuka matumizi ya mafuta na bidhaa zinazoweza kuharibu afya ya ngozi.

Akizungumza na SpotiLeo, Luizer amesema amewahi kupitia changamoto hiyo baada ya kushawishiwa na rafiki yake kutumia bidhaa iliyosababisha ngozi yake kuharibika.

Amesema ingawa kuacha matumizi ya bidhaa hiyo haikuwa rahisi, kwa sasa hali ya ngozi yake imeanza kuimarika na kurudi katika hali yake ya awali.

Kutokana na uzoefu huo, Luizer amewataka wanawake kutokubali shinikizo la kubadilisha mwonekano wa ngozi zao, akisisitiza umuhimu wa kujipenda na kuthamini uzuri wa asili.

“Akili za kuambiwa changanya na zako. Uzuri si kujichubua, ni wewe mwenyewe kukipenda na kuithamini ngozi uliyonayo,” amesema Luizer.

Ameongeza kuwa kila mtu anapaswa kuwa makini na bidhaa anazotumia kwenye ngozi na kuchagua njia salama za kuitunza badala ya kufuata ushawishi wa watu bila kufahamu madhara yanayoweza kujitokeza.

Related Articles

Back to top button