Chaka Chaka atoa wito kwa vijana kutumia sanaa kujenga fursa

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI nguli wa kimataifa kutoka Afrika Kusini, Yvonne Chaka Chaka, ametoa wito kwa jamii, vijana na wasanii kutumia sanaa, ubunifu na elimu kama nyenzo muhimu za kujenga fursa na kuchochea maendeleo.
Chaka Chaka ametoa ujumbe huo wakati akizungumza katika Mashariki Creative Economy Expo’26, yanayoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Msanii huyo amesema sanaa na ubunifu vina nafasi kubwa katika kuibua fursa kwa vijana na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii, akisisitiza umuhimu wa wasanii kuendelea kujifunza na kutumia vipaji vyao kwa manufaa ya jamii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wadau wa sanaa, akieleza kuwa kufanya hivyo kunaweza kusaidia kukuza sekta ya ubunifu na kuongeza fursa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Ushiriki wa Chaka Chaka katika maonyesho hayo umeongeza hamasa kwa washiriki, hususan vijana na wasanii wanaotafuta fursa kupitia sanaa na sekta ya uchumi wa ubunifu.
Mashariki Creative Economy Expo’26 inalenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya ubunifu, sanaa na utamaduni kwa ajili ya kuonesha vipaji, bidhaa za ubunifu, kubadilishana maarifa na kujenga fursa za kiuchumi.
Maonyesho hayo yameandaliwa na Culture and Development East Africa (CDEA).




