Ronaldinho arejea uwanjani akiwa na miaka 46

RAVENNA:NYOTA wa zamani wa Brazil na Barcelona, Ronaldinho Gaucho, anatarajiwa kurejea kucheza soka akiwa na umri wa miaka 46, zaidi ya miaka 10 tangu alipocheza mchezo wake wa mwisho wa kulipwa.
Ronaldinho ametambulishwa na klabu ya Ravenna inayoshiriki Serie C, daraja la tatu nchini Italia, ikiwa ni sehemu ya mpango wa klabu hiyo kuelekea msimu mpya. Mbali na kucheza, Ronaldinho pia atakuwa mmoja wa wanahisa wa Ravenna.
Mshindi huyo wa Ballon d’Or mwaka 2005 alicheza mchezo wake wa mwisho wa kitaaluma akiwa Fluminense ya Brazil mwaka 2015. Licha ya kutambulishwa rasmi na Ravenna, bado haijathibitishwa kama atashuka uwanjani, huku Ronaldinho mwenyewe akikiri kuwa hilo litategemea uamuzi wa kocha.
“Je, mtaniona nikicheza? Sijui, kocha ndiye anayejua,” amesema Ronaldinho.
Nyota huyo amesema amefurahia kurejea Italia na yupo tayari kusaidia kikosi hicho kupata mafanikio, huku akieleza kuwa moja ya malengo yake ni kufikisha mabao 300 katika soka la kulipwa.
Ravenna imepata hamasa kubwa kutokana na ujio wake, ikiwemo ongezeko la mauzo ya tiketi za msimu. Ripoti zinaeleza kuwa klabu hiyo imeuza tiketi za msimu 2,700, sehemu kubwa ikihusishwa na ujio wa Ronaldinho.
Ronaldinho alicheza mechi 97 kwa timu ya taifa ya Brazil na kufunga mabao 33. Katika historia yake, alitwaa Ballon d’Or, Kombe la Dunia 2002 pamoja na mataji ya ligi nchini Hispania na Italia.
Iwapo atashuka uwanjani akiwa na miaka 46, bado hatakuwa mchezaji mkongwe zaidi kuwahi kucheza soka, kwani rekodi hiyo inashikiliwa na Mjapani Kazuyoshi Miura, mwenye miaka 59.




