Msuva atua Newroz FC baada ya kung’ara Al Talaba

BAGHDAD: Mchezaji wa Taifa Stars, Simon Msuva, ameanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka baada ya kujiunga na klabu ya Newroz FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Iraq, akitokea Al Talaba FC ya nchini humo.
Uhamisho huo umekamilika kuelekea msimu mpya wa mashindano.
Mshambuliaji huyo wa Tanzania anajiunga na Newroz akiwa na rekodi nzuri kutoka Al Talaba, ambapo alikuwa mfungaji bora wa timu hiyo msimu uliopita kwa kufunga mabao tisa na kuwaacha nyuma wachezaji wenzake, akiwemo Habib Oueslati.
Kiwango alichoonesha Msuva kimekuwa moja ya sababu zilizomshawishi Newroz kumsajili kwa lengo la kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kuelekea msimu wa 2026/27, huku wakitarajia uzoefu wake utasaidia timu kufanya vizuri zaidi kwenye ligi.
Kwa miaka ya hivi karibuni, Msuva ameendelea kujijengea jina katika soka la Mashariki ya Kati baada ya kucheza katika klabu mbalimbali, huku akiendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Taifa Stars kutokana na uwezo wake wa kufunga na kutengeneza nafasi.
Uhamisho huo ni hatua nyingine muhimu katika safari ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32, ambaye sasa atakuwa na jukumu la kuiongoza Newroz katika harakati za kutafuta mafanikio kwenye Ligi Kuu ya Iraq msimu ujao.




