World Cup

Wadau wa soka wapinga uamuzi wa FIFA

..Trump atajwa kuingilia maamuzi

SHIRIKISHO la Soka Duniani (FIFA) limekumbwa na wimbi la ukosoaji kutoka kwa viongozi wa soka na wadau mbalimbali baada ya kusitisha adhabu ya kufungiwa mechi moja kwa mshambuliaji wa Marekani, Folarin Balogun, hatua iliyomruhusu kucheza dhidi ya Belgium katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia.

Uamuzi huo ulifanyika baada ya taarifa kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump, alimwomba Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kupitia upya kadi nyekundu aliyopewa Balogun.

Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA) imeeleza kuwa hatua hiyo imevuka mipaka ya kanuni za mchezo, ikisisitiza kuwa kufungiwa mechi moja baada ya kadi nyekundu ni adhabu ya moja kwa moja isiyopaswa kubadilishwa katikati ya mashindano.

Vilevile Chama cha soka Cha Ubelgiji kimesema ingawa FIFA imeegemea Kifungu cha 27 cha Kanuni za Nidhamu, Kifungu cha 66.4 kinaeleza wazi kuwa mchezaji anayepewa kadi nyekundu hukosa mechi inayofuata moja kwa moja.

Rais wa Chama cha soka cha Ujerumani, Bernd Neuendorf, ameitaka FIFA kutoa maelezo ya haraka kuhusu taarifa za mawasiliano kati ya Trump na Infantino, akisema ni muhimu kuondoa taswira ya kuingiliwa kwa siasa katika maamuzi ya michezo.

Kocha wa Belgium, Rudi Garcia, alikosoa uamuzi huo kwa kejeli akisema: “Sikujua kwamba Julai 5 kwenye Kombe la Dunia ni sawa na Aprili Mosi. Hatujitetei sisi, tunaitetea soka.”

Aliyekuwa Rais wa FIFA, Sepp Blatter, amesema kadi nyekundu hufutwa kwa kuzingatia sheria na ushahidi, si kwa simu za viongozi wa kisiasa, akionya kuwa uadilifu wa soka uko hatarini iwapo siasa zitaanza kuathiri maamuzi ya mchezo.

Kocha wa England, Thomas Tuchel, amesema ingawa anaamini tukio lenyewe halikustahili kadi nyekundu, uamuzi ulikuwa tayari umeidhinishwa na mwamuzi pamoja na VAR, hivyo alihoji ni nani aliyebadili uamuzi huo na kwa misingi gani.

Kwa upande wake, kocha wa Norway, Ståle Solbakken, amesema FIFA imefanya kosa kubwa ambalo linaweza kuathiri taswira ya Kombe la Dunia, akiongeza kuwa hata Marekani ikishinda dhidi ya Ubelgiji ushindi huo utaendelea kuzungumziwa kutokana na utata wa uamuzi huo.

 

Related Articles

Back to top button