LIGI kuu ya soka Tanzania Bara inaendelea leo kwa michezo mitatu huku mechi kivutio ikiwa kati ya Kagera Sugar na Simba.
Baada ya ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Geita Gold katika mchezo uliopita Simba ni mgeni wa Kagera Sugar kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.
Simba inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 37 baada ya michezo 16 wakati Kagera Sugar ipo nafasi ya 6 ikiwa na pointi 22 baada ya michezo 16.
Katika mchezo mwingine Geita Gold ina nafasi kurekebisha makosa ya kichapo hicho itakapoikaribisha Azam kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Azam ipo nafasi ya 3 ikiwa na pointi 36 baada ya michezo 16 wakati Geita Gold ipo nafasi ya 8 ikiwa na pointi 22 baada ya michezo 16.
Nayo Dodoma jiji baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya City katika mchezo uliopita itakuwa mgeni wa Tanzania Prison kwenye uwanja huo.
Dodoma Jiji ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 18 baada ya michezo 16 wakati Tanzania Prisons ipo nafasi ya 12 ikiwa pointi 15 baada ya michezo 16 pia.
Katika michezo ya ligi hiyo iliyopigwa Disemba 20 Yanga imeendeleza ubabe baada kuichapa Coastal Union mabao 3-0 huku Namungo ikishinda mabao 2-0 dhidi ya Ihefu wakati Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar zikitoka suluhu 0-0.




