Wabunifu wa mitindo wapigwa msasa elimu ya fedha

DAR ES SALAAM: WABUNIFU wa mavazi, wanamitindo na washonaji nchini wamepewa mafunzo ya elimu ya fedha yenye lengo la kuinua biashara zao, kuongeza ajira kwa vijana na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mafunzo hayo yalitolewa jana jijini Dar es Salaam katika Jukwaa la Mitindo Tanzania (Tanzania Fashion Forum), yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa taasisi za fedha na wadau wa tasnia ya ubunifu.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Jafari Hassanali, alisema tasnia ya mitindo inapaswa kubadilika kutoka kwenye kipaji na burudani na kuelekea kuwa biashara endelevu.
“Ubunifu tulionao lazima uendane na mifumo ya kibiashara ili kuushikilia na kuukuza uchumi wa Taifa. Tasnia ya mitindo ni sekta inayokua kwa kasi na ina uwezo mkubwa wa kutoa ajira, hasa kwa vijana,” amesema Hassanali.
Amewasisitiza wabunifu kutumia mikopo kwa uangalifu, akieleza kuwa mkopo ni nyenzo ya uwezeshaji na si mazoea.
“Unapokopa lazima ujue mkopo huo unaenda kufanya nini. Mkopo unapaswa kukamilisha oda au kuwekeza kwenye biashara, si kwa matumizi yasiyo na tija. Kukopa kwa ajili ya kula bata hakutakuza biashara,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa kukopa fedha kwa ajili ya kulipa madeni mengine bila kuwekeza ni kuua biashara badala ya kuikuza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Fashion Association Tanzania (FAT) na Muasisi wa Swahili Fashion Week, Mustapha Hassanali, alisema tasnia ya mitindo si suala la urembo pekee bali ni injini ya uchumi, ajira na utambulisho wa Taifa.
“Mitindo leo ni biashara, ni ajira, ni utambulisho wa Taifa na nafasi ya Tanzania katika dunia ya leo. Ubunifu bila mifumo, bila viwanda na bila miundombinu hauwezi kufika mbali,” amesema Mustapha.
Amesema kwa muda mrefu mitindo imeonekana kama maonesho pekee, badala ya sekta ya kiuchumi inayoweza kukuza biashara ndogo na za kati (SMEs), kuajiri vijana na kuongeza mapato ya Taifa.
“Dunia imetuonesha kuwa mitindo ya kimataifa ni sekta yenye thamani ya mabilioni ya dola. Nchi kama Italia, Uturuki na Morocco hazikufanikiwa kwa bahati mbaya, bali kwa kuitazama mitindo kama biashara na sekta ya viwanda,” ameeleza.
Mustapha amesema Tanzania ina vipaji vingi, lakini changamoto iliyopo ni kukosekana kwa mifumo madhubuti ya uzalishaji, masoko, mitaji na sera rafiki.
Ameongeza kuwa majadiliano hayo yanaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga uchumi wa viwanda, ajira zenye tija kwa vijana na kunufaika na masoko ya kikanda na kimataifa kupitia AfCFTA na mpango wa Made in Tanzania.
“Mustakabali wa ubunifu wa Tanzania hautajengwe kwa kusubiri. Utajengwa kwa vitendo, kwa kuunganisha serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na elimu,” amesema.




