Lulu Diva:Whozu si mpenzi wangu, ni rafiki yangu tu

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva Lulu Abas ‘Lulu Diva’ ameweka wazi msimamo wake kuhusu urafiki wake na msanii Whozu, ambaye aliwahi kuwa mpenzi wa Wema Sepetu, akikanusha vikali madai yanayosambaa mitandaoni kuwa amemsaliti rafiki yake kwa kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na Whozu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Lulu Diva amesema anasikitishwa na namna ambavyo wasanii wa kike mara nyingi huhusishwa na migogoro, usaliti na fitina zisizo na msingi, jambo linalochafua taswira ya kazi zao na utu wao.
“Kwanza, nasikitishwa sana namna ambavyo ‘brand’ zetu wasanii wengi wa kike zinahusishwa na mambo ya ugomvi, kusalitiana na mengine yasiyofaa. Wakati mwingine watu wametuvika vazi lisilotufaa,” ameandika Lulu Diva.

Ameeleza kuwa ameamua kulizungumzia suala hilo kwa mara ya mwisho, kwa heshima ya mashabiki wake na jamii kwa ujumla, akisisitiza kuwa ni wajibu wake kusema ukweli pale jina lake linapochafuliwa.
“Nimeona kwenye ukurasa wa Juma Lokole hapa Instagram ikisemwa kwamba ‘nimemzunguka rafiki yangu’. Hiki ni kitu kibaya na cha hovyo. Nimesema mara nyingi, lakini watu wanaendelea kulipotosha,” amesema.
Lulu Diva amesisitiza wazi kuwa Whozu ni rafiki yake wa muda mrefu, hata kabla hajaanzisha mahusiano na Wema Sepetu, na kwamba hawajawahi kuwa na uhusiano wowote wa kimapenzi.
“Kwa mara ya mwisho nasema: Mimi na Whozu hatukuwahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi. Urafiki wetu haukuanza baada ya mahusiano yake, na hauwezi kufa kwa sababu ya mahusiano hayo,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa wakati Whozu na Wema walipoanza mahusiano, alifurahi kama rafiki, lakini walipoingia katika changamoto zao za kimapenzi, kila mmoja alionekana kutaka awe upande wake, jambo alilolikataa kwa sababu wote ni marafiki zake.
“Mimi na aliyekuwa rafiki yangu tulipishana kwa sababu zingine kabisa ambazo sioni haja ya kuzieleza mtandaoni. Hili la Whozu naona ni katika kunitafutia ubaya mbele ya jamii,” ameongeza.
Akihitimisha, Lulu Diva amesema urafiki unaweza kufikia mwisho, lakini haupaswi kuwa chanzo cha uadui.
“Urafiki unaweza kufa, lakini usiwe mwanzo wa uadui. Kila mtu aendelee na maisha yake bila kutafutana ubaya,” ameandika.
Kwa upande wake, Wema Sepetu, alipofanyiwa mahojiano kwa njia ya simu na Juma Lokole, aliweka wazi maumivu yake, akieleza kuwa bado hana maelewano mazuri na Whozu, huku akidai alitarajia Lulu Diva awe upande wake kutokana na ukaribu waliokuwa nao.
“Lulu Diva alikuwa rafiki yangu wa karibu sana, tulifikia hatua ya kuitana my twin na my BFF, lakini sasa ameonekana kuwa karibu na Whozu. Inauma sana, lakini sina la kufanya,” alifunguka Wema.
Suala hilo limeendelea kuzua mjadala mpana mitandaoni, mashabiki wakitoa mitazamo tofauti kuhusu urafiki, mapenzi na mipaka yake katika maisha ya wasanii.




