AFCON

Vilio na vicheko kikosi cha Nigeria AFCON

LAGOS: TIMU ya taifa ya Nigeria (Super Eagles) inaingia kwenye michuano ya kombe la mataifa ya Afrika AFCON 2025 kikiwa na sura mpya na maamuzi ya kushangaza baada ya kocha Eric Chelle kutangaza kikosi cha wachezaji 28, ambacho kinajumuisha nyota wapya watano ambao hawajawahi kuichezea Super Eagles.

Kikosi hicho, kitakachoshiriki AFCON nchini Morocco kuanzia Desemba 21, kinaongozwa na washindi wa zamani wa tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika Ademola Lookman na Victor Osimhen, lakini pia kina sura mpya kama Ryan Alebiosu, Ebenezer Akinsanmiro, Tochukwu Nnadi, Usman Muhammed, na straika Salim Fago Lawal.

Chelle pia amemrudisha kikosini straika Paul Onuachu, ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali akiwa na magoli 11 akiwa na klabu yake ya Trabzonspor ya uturuki msimu huu kiwango kilichomfanya kuwa kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Uturuki. Onuachu alikuwa nje ya kikosi cha Nigeria kwa takribani miezi 18.

Hata hivyo, Nigeria inaingia AFCON ikiwa na wasiwasi wa majeraha baada ya kipa namba moja Stanley Nwabali kupata majeraha ya kifundo cha mguu na mkono. Nwabali hajacheza tangu Nigeria iondolewe kwenye ‘playoff’ za Kombe la Dunia mwezi uliopita, na kocha wake wa klabu nchini Afrika Kusini amesema hafikiri kama atakuwa tayari kwa michuano hiyo.

Super Eagles pia watamkosa beki muhimu Benjamin Fredericks na beki wa pembeni Ola Aina, wote wakiwa majeruhi, huku nahodha William Troost-Ekong akistaafu soka la kimataifa baada ya kushindwa kufuzu Kombe la Dunia.

Straika wa Wolverhampton Wanderers, Tolu Arokodare, ni mmoja wa waliokatwa kwenye orodha ya mwisho jambo lililowashangaza wengi.

Nigeria inaanza kampeni yake ya Kundi C dhidi ya Tanzania Desemba 23 mjini Fes, kabla ya kuvaana na Tunisia Desemba 27 na kumaliza hatua ya makundi dhidi ya Uganda Desemba 30.

Kikosi cha Nigeria – AFCON 2025
Makipa:
Stanley Nwabali (Chippa United), Amas Obasogie (Singida Black Stars), Francis Uzoho (Omonia Nicosia)
Mabeki:
Ryan Alebiosu (Blackburn Rovers), Chidozie Awaziem (Nantes), Semi Ajayi (Hull City), Calvin Bassey (Fulham), Igoh Ogbu (Slavia Prague), Bruno Onyemaechi (Olympiakos), Bright Osayi-Samuel (Birmingham City), Zaidu Sanusi (FC Porto)
Viungo:
Ebenezer Akinsanmiro (Pisa), Fisayo Dele-Bashiru (Lazio), Alex Iwobi (Fulham), Usman Muhammed (Ironi Tiberias), Wilfred Ndidi (Beşiktaş), Tochukwu Nnadi (Zulte Waregem), Raphael Onyedika (Club Brugge), Frank Onyeka (Brentford)
Washambuliaji:
Akor Adams (Sevilla), Samuel Chukwueze (Fulham), Cyriel Dessers (Panathinaikos), Chidera Ejuke (Sevilla), Salim Fago Lawal (Istra 1961), Ademola Lookman (Atalanta), Paul Onuachu (Trabzonspor), Victor Osimhen (Galatasaray), Moses Simon (Paris FC)

Related Articles

Back to top button