Man City yamtia ‘kiwewe’ Alonso

MADRID: PRESHA imezidi kumpanda kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso, kuelekea mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City utakaopigwa katika dimba la Bernabeu leo Jumatano saa 5 usiku.
Madrid imekuwa kwenye mwenendo wa kutatanisha, ikishinda mechi mbili pekee kati ya saba ilizocheza katika mashindano yote, ikiwemo kipigo cha 2-0 kutoka kwa Celta Vigo wikiendi iliyopita.
Hayajaishia hapo kabla ya kuukaribisha ugeni huu kutoka Etihad, vyombo vya habari nchini Hispania vimeripoti kuwa Alonso amepoteza udhibiti wa chumba chake cha kubadilishia nguo, madai ambayo ameyapinga.
“Hii ni timu, na tunasimama Pamoja. Katika soka, mtazamo unaweza kubadilika haraka sana, na tupo kwenye hatua hiyo sasa.” – Alonso amesema.
Hali ya mshambuliaji Kylian Mbappé imeongeza sintofahamu ndani ya kikosi, baada ya nyota huyo wa Ufaransa kufanya mazoezi kivyake Jumanne kutokana na kile kilichoripotiwa kuwa maumivu kwenye mguu wake wa kushoto.

Kwa upande wa Manchester City, kocha Pep Guardiola alionesha kumuelewa Alonso, akisema presha ya kazi ndani ya klabu kubwa kama Real Madrid ni ya kiwango cha juu mno.
“Barcelona na Real Madrid ni klabu ngumu zaidi kuifundisha kutokana na mazingira yake, Ni mazingira magumu, lakini yeye anayafahamu hiyo ndiyo hali halisi ya kuwa huko.” – Guardiola amesema.
Katika michezo mingine ya leo Jumatano, mabingwa watetezi Paris Saint-Germain watakuwa ugenini kwa Athletic Bilbao, Arsenal watavaana na Club Brugge, huku mabingwa wa Italia Napoli wakikabiliana na Benfica.




