
ZANZIBAR: SINGIDA Black Stars imejipanga upya kuelekea mchezo wake wa marudiano dhidi ya Stellenbosch FC, ikisisitiza kuwa chini ya Kocha Miguel Gamondi hawatarudia makosa yaliyowapotezea alama kwenye mchezo wa kwanza.
Timu hiyo ipo Zanzibar ambapo inaendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo huo utakaopigwa Jumapili.
Msemaji wa Singida Black Stars, Hussein Masanza, amesema maandalizi yanaendelea vizuri huku tathmini ya kina ya udhaifu uliojitokeza ikifanywa ili kuhakikisha wanarejea kwenye ushindani.
“Mchezo wa kwanza tulipoteza lakini tumepata mafunzo. Malengo yetu yalikuwa kuingia hatua ya makundi na kwa asilimia 100 tumefanikiwa. Hii ni fursa kubwa kwetu na tunaamini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri katika mechi tano zilizobaki,” alisema Masanza.
Amesema kikosi kipo kamili baada ya kurejea kwa kiungo Khalid Aucho, aliyekosekana kwenye mchezo wa awali, huku wachezaji wote wakiwa katika hali nzuri na tayari kuwakilisha nchi kwa ushindani mkali.
“Gamondi sio kocha anayefungwa mara mbili. Atafanyia kazi mapungufu na kuhakikisha tunapambana ipasavyo,” aliongeza.
Singida Black Stars inatarajia kutumia mchezo huo kama sehemu muhimu ya kujenga morali na kuonesha ubora wao katika michuano ya kimataifa.




