Simba yawatuliza mashabiki juu ya Bajaber

DAR ES SALAAM: WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamewatuliza mashabiki zake juu ya kutochezeshwa kwa mchezaji Mohamed Bajaber wakiwataka kuwa wavumilivu.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ahmed Ally, ametaja sababu zilizomfanya kiungo huyo kutoka Kenya, kushindwa kusafiri na kikosi hicho kuelekea nchini Mali ni kwa kuwa bado hajapona vizuri.
Simba wameifuata Stade Malien kwa ajili ya mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Kundi D, utakaochezwa Jumapili, Novemba 30.
Ahmed amesema uamuzi huo umefanyika kwa kuzingatia afya ya mchezaji, akibainisha kuwa Bajaber bado yupo kwenye hatua za mwisho za kupona majeraha yaliyomweka nje kwa miezi kadhaa.
“Niwaambie Wana Simba wasiwe na haraka, wasiwe na presha. Unaweza kumlazimisha mchezaji aingie uwanjani akapata jeraha kubwa zaidi. Maamuzi yanayofanyika ni sahihi kabisa,” amesema Ahmed.
Ameeleza kuwa mchezaji yeyote anayerejea kutoka kwenye majeraha makubwa anahitaji utaratibu maalum wa kumrudisha uwanjani ili kuhakikisha anarejea akiwa imara na salama.
“Mchezaji akitoka kwenye ‘injury’ kuna namna yake ya kurejea uwanjani. Kikubwa ni subira, atacheza tu na tutafurahia matunda yake. Kwa asilimia 99 anaendelea vizuri na ameanza kufanya mazoezi,” aliongeza.
Ahmed amesema licha ya maendeleo mazuri, bado ni mapema kumwingiza Bajaber kwenye mchezo mkubwa wa ushindani, kwani kukaa nje kwa zaidi ya miezi miwili au mitatu huathiri pia kujiamini (confidence) ya mchezaji.
Simba inahitaji ushindi muhimu ugenini baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Petro Atletico, na kikosi kinachotegemewa Mali kitakuwa bila kiungo huyo chipukizi aliyekuwa akifanya vizuri kabla ya jeraha.




