Becker ‘fiti’ kuwavaa Forest

LIVERPOOL: mabingwa watetezi wa Ligi kuu ya England Liverpool wanatarajia kumkaribisha tena kipa wao namba moja Alisson Becker dhidi ya Nottingham Forest Jumamosi, jambo litakalotoa ahueni mpya kwa kikosi cha Arne Slot baada ya kipindi kigumu kabla ya mapumziko ya kimataifa.
Mlinda mlango huyo wa Brazil anatarajiwa kuanza kwenye Uwanja wa Anfield baada ya kukosa mechi kwa takriban wiki saba kutokana na jeraha la msuli wa paja, wakati huu mabingwa hao wakitafuta kurejesha kasi yao ya ushindani.
Hata hivyo, Liverpool watakosa huduma za Conor Bradley na Florian Wirtz ambao wote walipata majeraha ya misuli wakiwa kwenye majukumu ya kimataifa, huku Bradley akitarajiwa kuwa nje kwa wiki tatu.

Liverpool wanashika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 18, nane nyuma ya vinara Arsenal. Mechi yao ya mwisho kabla ya mapumziko iliwashuhudia wakichakazwa mabao 3-0 dhidi ya Manchester City.
Kuhusu uwezekano wa kufanya usajili Januari, Slot amesema hilo si jambo analowaza kwa sasa. Akisema Kuna mechi nyingi sana kabla ya kufika January akisisitiza kuwa kuna mechi nyingi wanahitaji kushinda kabla ya kuwaza usajili.
Alipuuzia pia maswali kuhusu nafasi ya timu yake kutetea taji la Premier League.
“Hatufikirii wala kuzungumzia hilo. Hata msimu uliopita tulipokuwa kileleni, tulisisitiza tu mchezo unaofuata. Msimamo wa ligi ni bora kuuangalia baada ya mechi 38, na chaguo la pili ni baada ya mechi 19. Tutaona tupo wapi kufikia hapo,” – alisema kocha huyo Mholanzi.




