Nyumbani

Manara azitakia heri Simba, Yanga kimataifa

DAR ES SALAAM: DIWANI wa Kata ya Kariakoo, Haji Manara, amezitakia heri timu zote nne Simba, Yanga, Singida Black Stars na Azam zifanye vizuri katika michuano ya makundi Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Leo, Manara ambaye aliwahi kuwa Msemaji wa klabu kongwe Simba na Yanga alisema kwa kuwa yeye ni shabiki wa Yanga basi anawahimiza mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar Jumamosi kuiunga mkono timu hiyo.

Yanga itamenyana na AS FAR Rabat ya Morocco huku Manara akisema mechi hiyo inapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa.

“Ni mechi ngumu” ambayo itahitaji utashi na kujitolea kutoka kwa wachezaji.

“Naomba wananchi twende kwa amani, tuwaheshimu wageni, na tuisapoti Yanga. Ni mechi kubwa — wachezaji wajaribu kwa moyo wote; nina imani kuwa watapata matokeo mazuri,” alisema Manara.

Alisema: “Simba, Azam na Singida tuwatakie kila la heri. Kariakoo ni chimbuko la Azam, Simba na Yanga. Hii ni fursa ya kuonesha kuwa sisi sote ni sehemu ya familia ya soka — bila ubaguzi,” alisema.

Simba itacheza Jumapili dhidi ya Petro Atletico de Angola huku Azam FC na Singida zikianzia ugenini dhidi ya AS Maniema ya DR Congo na CR Belouzdad ya Algeria.

Related Articles

Back to top button