Nyumbani

Kapombe: Tunakwenda kupigania heshima ya Taifa

DAR ES SALAAM: BEKI wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Shomari Kapombe, amesema wachezaji wote walioko kambini wako tayari kuhakikisha timu inafanya vizuri katika michezo ijayo, ikiwemo ule wa kirafiki dhidi ya Kuwait.

Akizungumza akiwa kambini, Kapombe alisema dhamira ya wachezaji ni moja kuhakikisha wanafanya kila kitu kwa ufanisi ili kufikia malengo ya timu.

“Kama wachezaji tuko hapa kwa ajili ya kuhakikisha taifa letu linafanya vizuri. Tuko hapa kuhakikisha kila kitu ambacho mwalimu anatupatia tunakifanya kwa asilimia 100 ili kufikia malengo,” alisema Kapombe.

Aliongeza kuwa maandalizi ya mchezo wa kirafiki yanaendelea vizuri na anaamini yatakuwa sehemu muhimu ya maandalizi kuelekea michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

“Tunaendelea na maandalizi, tumeingia kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Kuwait. Nina imani utakuwa mchezo mzuri na wenye maandalizi bora kuelekea Afcon.

Alisema kwa sasa kuna benchi jipya la ufundi, wapo tayari kwa maelekezo yao ili kufanya vizuri kwenye mchezo huo.

Mchezo wa kirafiki kati ya Tanzania na Kuwait unatarajiwa kuchezwa jijini Cairo, Misri, Novemba 15, mwaka huu kama sehemu ya maandalizi ya Stars kuelekea fainali za AFCON.

Related Articles

Back to top button