Kwingineko

Bellingham, Foden warudi kikosini England, Scott nae ndani

LONDON: KOCHA wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, amemrejesha kikosini Mshambuliaji wa Real Madrid Jude Bellingham na Kiungo wa Phil Foden kwenye kikosi chake cha michezo ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Serbia na Albania wiki ijayo, huku kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, akipata wito wake wa kwanza kujiunga na kikosi cha wakubwa.

Tuchel amepuuza wito wa kumjumuisha mshambuliaji wa Brighton, Danny Welbeck, huku kiungo mshambuliaji Jack Grealish anayecheza kwa mkopo Everton akitokea Manchester City na beki wa kulia Trent Alexander-Arnold wakikosa nafasi.

Bellingham, anayechezea Real Madrid, alikosa michezo ya mwezi Oktoba kutokana na jeraha la bega, wakati Foden wa Manchester City alikuwa hajaichezea England tangu mwezi Machi walipokutana na Latvia.

Scott, mwenye umri wa miaka 22, alikuwa sehemu ya kikosi cha vijana wa England (U21) kilichotwaa ubingwa wa Ulaya. Ameshacheza mechi zote 10 za Bournemouth kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu, akifunga bao moja na kusaidia klabu hiyo kushika nafasi ya tano kwenye msimamo.

Wachezaji wengine waliorejea kikosini ni kipa wa Newcastle, Nick Pope, beki wa Manchester City Nico O’Reilly, na kiungo wa Crystal Palace Adam Wharton. Walioachwa kutoka kikosi kilichopita ni Morgan Gibbs-White, Myles Lewis-Skelly, Ruben Loftus-Cheek, James Trafford na Ollie Watkins.

England tayari wamefuzu Kombe la Dunia la 2026 baada ya ushindi mnono dhidi ya Latvia mwezi Oktoba. Watakuwa wenyeji wa Serbia mnamo Novemba 13, kabla ya kusafiri kwenda Albania siku tatu baadaye kwa mchezo wao wa mwisho wa Kundi K. Hizo zitakuwa mechi zao za mwisho za mashindano kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Canada, Mexico na Marekani.


______________
Kikosi kamili cha England:

Makipa: Dean Henderson (Crystal Palace), Jordan Pickford (Everton), Nick Pope (Newcastle United)

Mabeki: Dan Burn (Newcastle United), Marc Guehi (Crystal Palace), Reece James (Chelsea), Ezri Konsa (Aston Villa), Nico O’Reilly (Manchester City), Jarell Quansah (Bayer Leverkusen), Djed Spence (Tottenham Hotspur), John Stones (Manchester City)

Viungo: Elliot Anderson (Nottingham Forest), Jude Bellingham (Real Madrid), Jordan Henderson (Brentford), Declan Rice (Arsenal), Morgan Rogers (Aston Villa), Alex Scott (Bournemouth), Adam Wharton (Crystal Palace)

Washambuliaji: Jarrod Bowen (West Ham United), Eberechi Eze (Arsenal), Phil Foden (Manchester City), Anthony Gordon (Newcastle United), Harry Kane (Bayern Munich), Marcus Rashford (Barcelona – mkopo kutoka Manchester United), Bukayo Saka (Arsenal)

Related Articles

Back to top button