Kwingineko

Ajax yamfuta kazi Heitinga

AMSTERDAM: MABINGWA wa kihistoria wa ligi kuu ya Uholanzi Eredivisie Ajax Amsterdam wamemfuta kazi kocha wake John Heitinga kufuatia mwanzo mbaya wa msimu, ambao umehusisha vipigo vinne vizito mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Klabu hiyo imethibitisha kwamba Fred Grim ataongoza timu kwa muda, huku kocha msaidizi Marcel Keizer naye akifurushwa. Pia Mkurugenzi wa ufundi wa Ajax, Alex Kroes, alisema atajiuzulu kabla ya mkataba wake kuisha mwishoni mwa msimu iwapo klabu itapata mbadala anayefaa.

Ajax imeshinda mechi tano pekee kati ya 11 kwenye Eredivisie msimu huu na inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, lakini iko mkiani kwenye msimamo wa Ligi ya Mabingwa, hali inayodhihirisha miezi michache ya sintofahamu ndani ya klabu hiyo.

“Ni uamuzi mgumu. Lakini tukitazama miezi michache iliyopita, mambo hayajaenda kama tulivyotarajia. Hatukuona maendeleo ya kutosha na tumepoteza pointi nyingi bila sababu za msingi.

“Tunatambua kwamba kocha mpya anahitaji muda kufanya kazi na kikosi kipya, tumempa John nafasi hiyo, lakini tunaamini ni bora kumpa mwingine majukumu ya kuongoza timu. Tunatarajia kutangaza kocha mpya hivi karibuni.”

Heitinga mwenye miaka 41, ni mchezaji wa zamani wa Ajax aliyeichezea klabu hiyo mechi 218 kabla ya kuwa kocha wa timu ya vijana.

Aliwahi pia kushika nafasi ya ukocha wa muda mwaka 2023 baada ya kufukuzwa kwa kocha Alfred Schreuder, kisha akawa kocha msaidizi kwa David Moyes West Ham na baadaye Arne Slot Liverpool, ambapo alisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Premier League msimu uliopita.

Alirejea Ajax mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuondoka kwa kocha wa Muitaliano, Francesco Farioli. Ajax itarejea dimbani Jumapili watakapomenyana ugenini na Utrecht.

Related Articles

Back to top button