Kwingineko

Kisa Foden, Guardiola amtwisha zigo Tuchel

MANCHESTER: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola, amemwagia sifa kiungo wa klabu hiyo Phil Foden baada ya kuwa katika kiwango bora na kuchangia mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-1 wa klabu hiyo dhidi ya Borussia Dortmund kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na kupendekeza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 arejeshwe kwenye timu ya taifa.

Foden amekuwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya England tangu mwezi Machi mwaka huu, na kocha Guardiola anaamini kiwango cha sasa cha kiungo huyo ni wazi kwamba ana nafasi kubwa ya kurejea kwenye mipango ya kocha wa timu ya England Thomas Tuchel

Tuchel anatarajiwa kutangaza kikosi kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia wiki ijayo kujiandaa kwa mechi dhidi ya Serbia na Albania. Alipoulizwa kama kiwango cha Foden kinaweza kumsaidia kurejea kwenye timu ya taifa, Guardiola alijibu kwa maneno yenye hekima lakini yenye maana pana

“Thomas (Tuchel) ni mwerevu na mwenye uzoefu mkubwa, anajua vizuri nini timu ya taifa inahitaji. Anajua ubora wa Phil. Lakini timu ya taifa ni tofauti unakuwa na muda mfupi, na si timu inayokutana kila siku,”

“Lakini hebu tuwe wakweli, hakuna mtu nchini England wala duniani kote ambaye hajui ubora wa Foden. England ina wachezaji wengi wazuri, ndiyo maana Phil anatakiwa ajisukume zaidi, awe bora na bora zaidi, ili atakapoitwa aseme: ‘Sawa, sasa ni wakati wangu kuonesha ubora wangu’.” – alisema Pep

Related Articles

Back to top button