BurudaniMuziki

Nyota wa Muziki wa Neo-Soul D’Angelo azikwa Virginia

VIRGINIA: DUNIA ya muziki imeendelea kuomboleza kifo cha Michael Eugene Archer maarufu D’Angelo, mkongwe wa muziki wa R&B na neo-soul, ambaye amezikwa rasmi katika jimbo lake la nyumbani, Virginia, Marekani.

Katika ibada ya mazishi iliyohudhuriwa na familia, marafiki na wasanii wenzake, makundi yake ya zamani The Soultronics na The Vanguard walifanya maonesho maalum ya muziki kwa heshima yake.

Msanii mkongwe Stevie Wonder pia alitumbuiza kwa nyimbo za kiroho ‘If It’s Magic, The Lord’s Prayer’ na ‘As’, akishirikiana na vikundi hivyo na mpiga kinanda wa harp Brandee Younger.

Mshindi huyo wa tuzo ya Grammy, ambaye jina lake halisi lilikuwa Michael Eugene Archer, alifariki dunia mwezi uliopita akiwa na miaka 51 kutokana na saratan ya kongosho.

Familia yake ilitoa taarifa yenye huzuni ikisema:

“Nyota inayong’aa zaidi katika familia yetu imezimika katika dunia hii. Baada ya mapambano marefu na ya ujasiri dhidi ya saratani, tunasikitika kutangaza kwamba Michael D’Angelo Archer, anayejulikana duniani kama D’Angelo, ameondoka Oktoba 14, 2025. Tumehuzunishwa sana, lakini tunashukuru kwa urithi wa muziki wa kipekee aliotuachia.”

Familia pia iliwataka mashabiki kuheshimu faragha yao wakati huu wa maombolezo, lakini wakawahimiza wote kuungana nao katika kusherehekea zawadi ya muziki aliyouacha duniani.

Baada ya kifo chake, salamu za rambirambi zilimiminika kutoka kwa nyota wakubwa, akiwemo Beyoncé, ambaye alimtaja kama “mbunifu wa muziki wa neo-soul.”

Kupitia tovuti yake rasmi, Beyoncé aliandika: “Pumzika kwa amani, Michael Eugene Archer, anayejulikana na ulimwengu wa muziki kama D’Angelo. Tunakushukuru kwa sauti yako nzuri, muziki wako, kipaji chako cha kupiga piano, na ubunifu wako. Wewe ndiye ulieleta mageuzi makubwa kwenye muziki wa rhythm and blues. Hatutakusahau kamwe.”

Binti yake, Imani Archer, alielezea majonzi makubwa kupitia ukurasa wake wa Instagram, akisema hawezi kuamini kilichotokea.

“Baba mpendwa, hakuna maneno ya kuelezea huzuni hii kubwa. Niko katika hali ya mshangao na kutokuamini. Wewe ulikuwa mshabiki wangu mkubwa, mlinzi wangu, chanzo changu kikuu cha muziki, na baba bora zaidi mtu yeyote angeweza kuwa naye.”

Mazishi hayo yalikuwa ya heshima kubwa, yakionesha jinsi D’Angelo alivyoacha alama isiyofutika katika historia ya muziki wa dunia.

D’Angelo (1974 – 2025) atakumbukwa kama sauti ya roho, mbunifu wa mtindo wa neo-soul, na msanii ambaye muziki wake uliunganisha vizazi na kugusa mioyo ya mamilioni.

“Kupitia muziki wake, roho yake itaendelea kuimba milele.”

Related Articles

Back to top button