De Bruyne amaliza utata Napoli

NAPLES: KIUNGO wa kati wa Napoli Kevin De Bruyne ametolea majibu utata juu ya jinsi alivyochukulia kufanyiwa mabadiliko mara mbili baada ya kutoa asisti mbili katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sporting Lisbon kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa kuamkia leo.
De Bruyne hakuficha kutoridhishwa kwake alipotolewa wakati Napoli ikipoteza mbele ya AC Milan wikiendi iliyopita, jambo ambalo lilimfanya kocha Antonio Conte kuonya, “Natumai alikasirishwa na matokeo. Kwa sababu ikiwa alikerwa na kitu kingine, anashughulika na mtu tofauti.”
Baadaye Conte alisema kwamba yeye na De Bruyne walikuwa wameweka mambo sawa na ‘staa’ huyo wa zamani wa Manchester City alionekana kuwa tayari kwa kipute dhidi ya Sporting.
“Hakukuwa na tatizo lolote. Mimi ni mshindi. Nataka kucheza soka. Nataka kuleta mabadiliko, Kila kitu kilichosemwa. Nawahakikishia hakuna tatizo” – De Bruyne alisema.
De Bruyne alihusika na mpira ulitengeneza bao la kwanza la Rasmus Hojlund kwa Napoli na kisha akatoa asisti nyongine kwa goli la kichwa la Hojlund lililorejesha furaha ya Napoli kipindi cha pili.
“Kevin ni gwiji wa huu mchezo, Kwangu mimi, kila wakati anapopata mpira, ni kama ananiambia nenda katafute nafasi. Najawa shukrani sana kucheza na mchezaji kama huyu.” – Hojlund alisema.