Kwingineko

Tielemans nahodha mpya Ubelgiji

BRUSSELS: TIMU ya taifa ya Ubelgiji imemchagua kiungo wa Aston Villa Youri Tielemans kuwa nahodha wao licha ya kikosi hicho cha kocha Rudi Garcia kuwa na idadi ya wachezaji kadhaa wenye uzoefu zaidi kikosini na majina makubwa.

Tangu Garcia alipoanza kuifunda timu hiyo mapema mwaka huu, alizungusha litambaa cha unahodha huku akisema anatafuta kiongozi sahihi wa kikosi hicho lakini jana Jumatano alimtangaza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 kama nahodha wa kudumu.

“Youri Tielemans atakuwa nahodha wetu wa kudumu. Tumezungusha kitambaa cha unahodha kwa muda mrefu, lakini sasa uamuzi umefikiwa. Ana uhusiano mzuri na kila mtu kikosini”.

“Anafurahia umoja uliopo ndani. Ingawa wengine wanasalia kuwa viongozi muhimu, kama Kevin De Bruyne, Thibaut Courtois, na Romelu Lukaku lakini tunampa kitambaa Youri” – Garcia aliuambia mkutano na waandishi wa habari usiku wa kuamkia Alhamisi.

Kwa upande wake Tielemans amesema anachukulia uteuzi huo kama heshima kubwa kwake huku akiahidi mabadiliko makubwa ya uongozi wa kikosi hicho na kuendeleza ushirikiano na manahodha waliopita.

“Kuna vitu vichache vizuri kwenye tasnia kuliko hivi. Kulikuwa na majina matano na mimi nimechaguliwa. Haingeleta tofauti yoyote kwangu. Nitakuwa yule yule wakati wote, tutashirikiana, hiyo ni uhakika,nafasi hii haitanibadilisha.” – amesema

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button