Nyumbani

Simba yafaidi kambi Misri, Matola atoa neno

DAR ES SALAAM: KOCHA Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kimenufaika kwa kiasi kikubwa na kambi ya mazoezi waliyoiweka nchini Misri, akibainisha kuwa maandalizi hayo yamewapa picha halisi ya wachezaji kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC na mashindano ya kimataifa.

“Kiukweli tumeridhika, kitu ambacho tulikihitaji kwenye kambi tumekipata. Picha yote halisi ya wachezaji tumeiona na tumeweza kufaidika kwa kucheza michezo ya kirafiki,” amesema Matola.

Katika kambi hiyo, Simba ilipata nafasi ya kucheza michezo kadhaa ya kirafiki ikiwemo dhidi ya Wadi Degla ya Misri waliyoshinda mabao 2-1 kabla ya kumalizia maandalizi kwa kuvaana na mabingwa wa Liberia, FS Fassel, ambapo walitoka sare ya 1-1.

Matokeo hayo yametoa picha ya changamoto na maeneo ya kuboresha ndani ya kikosi hicho, jambo lililosaidia benchi la ufundi kubaini uimara na mapungufu ya wachezaji, na kujiweka tayari kwa mashindano mbalimbali msimu huu.

“Niwaambie wanasimba waje kutusapoti, kitu ambacho tumekitengeneza huku nina imani ni kikubwa sana. Nafikiri picha ya Simba halisi wataiona kwenye Simba Day. Tuko vizuri na tumeweza kufanikisha kambi ya Misri,” aliongeza Matola.

Kikosi cha Simba kinatarajia kurejea Dar es Salaam leo tayari kwa Simba Day.

Simba Day yenyewe itafanyika Septemba 10, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo kutakuwa na burudani, utambulisho wa kikosi kipya na kutoa heshima kwa nyota waliotumikia klabu akiwemo nahodha Jonas Gellard Mkude anayestaafu baada ya miaka 15 na mshambuliaji John Bocco.

Related Articles

Back to top button