Nyumbani

Serikali kuwavuta wadhamini wa michezo

DAR ES SALAAM:NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema serikali inaendelea kuhakikisha mazingira rafiki kwa wawekezaji na wadhamini wa michezo ili kuvutia uwekezaji zaidi katika klabu na mashindano.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba mpya wa udhamini wenye thamani ya Shilingi Bilioni 21.75 kati ya Yanga na SportPesa, Mwinjuma alisema udhamini huo umesaidia siyo tu klabu hiyo, bali pia ustawi wa michezo kwa ujumla.

Mwinjuma amebainisha kuwa michezo huchangia sio burudani pekee, bali pia maendeleo ya kiuchumi, kukuza afya za Watanzania, na kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.

“Tunataka kuendelea kuwa na makampuni mengi kama SportPesa, benki, na mashirika mengine ambayo yanaona fursa katika michezo yetu. Huu ni uwekezaji ambao mmepata faida nao na mmewasaidia wachezaji na klabu kukua,” ameongeza.

Amesema ushirikiano wa muda mrefu kati ya SportPesa na Yanga ni mfano mzuri wa jinsi sekta binafsi inavyoweza kuchangia maendeleo ya michezo nchini.

Amesema kuwa Wizara ipo tayari kushirikiana na wadhamini wote kuhakikisha michezo inakua na kufikia viwango vya kimataifa.

Related Articles

Back to top button