Kudus avutiwa na kocha akitua Spurs

LONDON, Mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana Mohamed Kudus amesema amevutiwa na project ya kocha Thomas Frank mchezaji huyo akisaini mkataba wa muda mrefu Tottenham Hotspur kutoka West Ham United alikodumu kwa misimu miwili.
Taarifa iliyotolewa na Spurs wakati wa utambulisho wake imemnukuu Kudus akisema uwezo wa kipekee wa Thomas Frank wa kukuza na kuendeleza wachezaji ni moja ya sababu za nyota huyo kuhamia katika viunga vya London kaskazini
“Moja ya sehemu muhimu kwa nini nilikuja hapa ni ‘Project’ ya klabu na jinsi meneja (Thomas Frank) anavyoiona na kuiendeleza chini yake” Kudus alisema katika taarifa hiyo.
“Kwa historia ya alikotoka, nimeona kiwango cha vipaji alichokuza hadi kuwa wachezaji wazuri. Ni ishara kubwa na ya wazi kwanini nilitaka kufanya kazi chini yake pia.”
Kudus alijiunga na West Ham kutoka Ajax Amsterdam mwaka 2023 kwa takriban euro milioni 40 (Shilingi bilioni 9.1 za kitanzania wakati huo) na kufunga mabao 13 na kutoa asisti 12 katika misimu miwili ya ligi akiwa na klabu hiyo.
Ingawa alifunga mabao matano pekee katika msimu mbaya ya ligi kwa West Ham msimu uliopita nguvu na uwezo wake wa kupiga chenga vinaweza kumfanya kuwa nyenzo muhimu kwa kocha Frank, ambaye anatarajiwa kutumia mfumo ule ule wa mashambulizi ya kushtukiza aliyoutumia akiwa Brentford.