Enrique akwepa swali la Mbappe

EAST RUTHERFORD, Kocha wa mabingwa wa Ulaya Paris St Germain, Luis Enrique amekataa kulinganishwa kikosi chake kilichoshinda Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliomalizika na timu ambayo hapo awali ilimjumuisha mshambuliaji wa Real Madrid Kylian Mbappe.
Luis Enrique aliuambia mkutano na waanahabari kuwa ni mambo ya kizamani kumzungumzia Mbappe alipoulizwa ikiwa PSG yake ni timu bora sasa hivi bila Mbappe kuliko walipokuwa na nahodha huyo wa Ufaransa kwenye kikosi chao kabla hajatimkia Real Madrid mwaka jana.
“Hili swali ni kuhusu ‘mambo ya zamani’ na siko hapa kuzungumzia yaliyopita, akili yangu inafikiria tu siku zijazo” alisema Enrique
Kocha huyo Mhispania alikiri kuwa kucheza dhidi mchezaji wake huyo wa zamani kunaongeza ladha kwenye mechi hiyo akisema kwamba ni motisha ya ziada kucheza dhidi ya timu yenye mafanikio zaidi duniani.
PSG italazimika tena kukabiliana na hali mbaya ya hewa ya jimbo la New Jersey, kwani mchezo wao utapigwa mchana kwa joto kali baada ya joto katika mchezo wa Chelsea na Fluminense kupanda hadi nyuzi joto 35 na unyevu wa zaidi ya 54%.
“Tunazoea kucheza katika mazingira haya, kwa sababu hiyo imekuwa kawaida wakati wa Kombe hili la Dunia la Klabu. tutacheza kama kawaida yetu. Najua hali ya hewa haitaruhusu mchezo mzuri kwa sababu ni vigumu kucheza katika joto la namna hiyo. Na hii ni kwa timu zote mbili.” – Luis Enrique amesema.
Mshindi wa mchezo kati ya PSG na Real Madrid atavaana na Chelsea ambayo imeifurusha Fluminense katika michuano hiyo jana usiku katika mchezo wa fainali Jumapili mjini New Jersey.