Sekta binafsi ina mchango sekta ya sanaa

SEKTA binafsi imeendelea kuwa na mchango katika kuendeleza sekta ya sanaa, michezo na ubunifu kwa kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/26.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwaka 2024/25 jumla ya kampuni 19 zilipewa kandarasi za kutekeleza miradi mbalimbali ya sekta ya habari, sanaa, michezo na ubunifu.
Kati ya kampuni hizo, 10 ni za Watanzania na 9 ni za nje. Vilevile, sekta binafsi imeendelea kushiriki katika kuendeleza na kukuza vipaji vya michezo ambapo jumla ya klabu za michezo 692 zimeanzishwa.
Pia, sekta binafsi inashiriki katika kukuza vipaji na ubunifu katika sanaa mbalimbali. Ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo umechangia ongezeko la ajira, kipato, kuchochea uchumi na kujenga uwezo wa sekta binafsi ya ndani.




