Neymar arejea Santos na ‘gundu’

SANTOS: WINGA wa zamani wa FC Barcelona, PSG, timu ya taifa ya Brazil na sasa klabu ya Santos ya Brazil, Neymar da Silva Santos Júnior ‘Neymar’ amerejea uwanjani baada ya majeraha ya paja yaliyomuweka nje ya uwanja kwa mwezi mmoja huku usiku wa kuamkia leo akishuhudia klabu yake hiyo ikiondoshwa kwenye michuano ya Copa do Brasil baada ya kufungwa penalti 5-4 penalti dhidi ya CRB baada ya sare ya 0-0.
Taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa, Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 bado hajui hatma yake katika klabu hiyo iliyomlea alikorejea baada ya kuichezea Al-Hilal ya Saudi Arabia, huku mkataba wake katika timu hiyo ya Brazil ukitamatika Juni 30.
Neymar amekuwa akiandamwa na majeraha mabaya mara kwa mara, na aliondoka uwanjani akilia mwezi uliopita baada ya kupata jeraha lake la pili kubwa mwaka huu pekee. Hata hivyo Neymar hakutoa maelezo ya kutosha alipoulizwa kuhusu hatma yake klabuni hapo na jibu pekee alolotoa lilikuwa ni “bado sijui”
Santos, ambao wametoa sare na CRB katika mechi zote mbili za raundi ya tatu ya Copa do Brasil kwa sasa wako katika nafasi ya pili kwenye mkia wa msimamo wa ligi kuu ya Brazil Serie A, wakiwa wamepoteza mechi sita kati ya tisa za kwanza walizocheza msimu huu.




