Nyumbani
Yao aanika magumu anayopita

DAR ES SALAAM:BEKI wa kulia wa Yanga, Yao Kouassi Attohoula, amesema maisha ya mchezaji wa mpira si ya mafanikio tu kila wakati, bali kuna nyakati ngumu ambazo mchezaji hukutana nazo.
Yao ameweka picha akiwa hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti, sambamba na ujumbe unaoonesha namna anavyopitia maumivu kwa sasa.
Katika ujumbe wake, Yao ameandika:
“Tuwe na utamaduni wa kukubali kwamba si kila kitu katika maisha yetu kinapaswa kuwa chepesi au kizuri kila wakati.Kushindwa kweli kunakuwepo na nyakati ngumu pia zina nafasi katika maisha yetu. Kila mtu anaweza kupitia changamoto, yote ni suala la muda na kufanya kazi kimya kimya ili kurudi kileleni.”
Beki huyo amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na goti la kushoto, na tayari amefanyiwa upasuaji tangu wiki iliyopita nchini Tunisia.
Awali, Yao alikuwa akisumbuliwa na kifundo cha mguu pamoja na nyama za paja, matatizo yaliyomsababisha kukosa mechi kadhaa, ingawa baadaye alipona.
Changamoto hii inamkumba beki huyo wakati mkataba wake ukiwa unaelekea ukingoni, hali inayozua maswali kuhusu mustakabali wake ndani ya kikosi cha Yanga.