
DAR ES SALAAM: MWIGIZAJI na msanii maarufu Hamilton William, anayejulikana zaidi kama Ngoma Nagwa, ameweka nadhiri ya kuendelea kung’ara katika sanaa mpaka mwisho wa nguvu zake, akisisitiza kuwa hatorudi nyuma kamwe.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram leo, ikiwa ni siku yake ya kuzaliwa, Ngoma Nagwa amechapisha ujumbe mzito uliojaa maono na matumaini mapya. “Siyo tu siku ya kuzaliwa kwangu, ni siku ya kuzaliwa kwa nguvu mpya ndani yangu – nguvu ya kusimama jukwaani bila hofu, kuandika stori zenye roho, na kuifanya sanaa yangu isiguse tu mioyo, bali iitikise dunia,” ameandika.
Akiendelea kuelezea azma yake, Ngoma amesema: “Sijazaliwa kuwa wa kawaida. Nimeumbwa kubadilisha maisha kupitia kipaji changu. Leo naweka nadhiri sitarudi nyuma, nitang’ara mpaka tone la mwisho la jasho langu. Asante Mama yangu.”
Kwa miaka mingi, Ngoma Nagwa ameonesha uwezo wa kipekee si tu katika uigizaji bali pia kwenye muziki, akitumia kipaji chake kugusa hisia za watu na kuhamasisha mabadiliko ya kijamii. Ujumbe wake wa leo unadhihirisha dhamira yake ya kuendelea kupigania ndoto zake bila woga, licha ya changamoto nyingi katika tasnia ya sanaa.