Aziz Ki na Yanga ndio basi tena

DAR ES SALAAM:KIUNGO mahiri wa Klabu ya Yanga, Stephane Aziz Ki, ameaga rasmi maisha ya soka Tanzania baada ya kuondoka nchini kuelekea Morocco, anatarajiwa kujiunga na klabu ya Wydad AC.
Kiungo huyo raia wa Ivory Coast anatarajiwa kutua katika jiji la Casablanca leo, Jumatatu ya Mei 19, kwa ajili ya kukamilisha usajili wake wa miaka miwili na miamba hiyo ya Morocco.
Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Yanga zinaeleza kuwa mazungumzo baina ya pande hizo mbili yalifikia tamati baada ya Wydad AC kuwasilisha ofa ya kuvutia, ambayo ilikubaliwa na viongozi wa Yanga.
Inaelezwa kuwa mchezaji huyo atalipwa kiasi kikubwa zaidi ya kile alichokuwa akipokea akiwa na Wananchi.
Chanzo cha karibu na mchezaji huyo kimethibitisha kuwa Aziz Ki tayari ameaga wachezaji wenzake, huku mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya JKT Tanzania ikiwa ni ya mwisho kwake akiwa katika jezi ya Yanga.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Alex Ngai, alikiri kuwepo kwa mazungumzo baina ya Yanga na klabu nyingine kubwa(hakuitaja), akieleza kuwa kila kitu kiko katika hatua nzuri.
“Ni kweli kuna mazungumzo ambayo yanaendelea baina ya klabu ya Yanga na klabu nyingine, mambo yakiwa vizuri Aziz Ki anaweza kuondoka Yanga na kwenda kupata changamoto nyingine,” amesema Ngai.
Usajili huu unakuja kama pigo kwa mashabiki wa Yanga ambao walimwona Aziz Ki kama mhimili wa kikosi, lakini pia ni fursa kwa nyota huyo kuonyesha uwezo wake kwenye jukwaa kubwa zaidi barani Afrika.