Goli la Mama laitikisa Samia Serengeti Music Festival
Mashabiki wa Yanga wavuna milioni moja

DAR ES SALAAM: SIO klabu ya Simba pekee inayovuna “Goli la Mama” kupitia michuano ya kimataifa, hata katika tamasha la Samia Serengeti Music Festival linalofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, mashabiki wa Yanga nao wamejizolea kitita cha shilingi milioni moja baada ya kuibuka kidedea dhidi ya Simba.
Katika mchezo wa mpira wa miguu uliowakutanisha mashabiki wa timu hizo kongwe za Tanzania, mshindi alipata zawadi ya shilingi 1,000, 000 na wapili alivuna 500,000, huku jumla ya zawadi zilizotolewa zikifikia milioni moja na laki tano.
Hali hiyo imeonesha kuwa dhana ya “Goli la Mama” sasa imevuka mipaka ya michuano ya kimataifa na kuhamia pia katika matamasha ya burudani na michezo ya ndani.
Kawaida, “Goli la Mama” tulizoea kulisikia likihusishwa na timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa kama vile Kombe la Shirikisho la Afrika, ambapo kwa sasa ni Simba pekee inayowakilisha nchi katika hatua hiyo.
Katika tamasha hili lililopambwa na michezo na burudani za muziki, Yanga waliandika historia kwa kuondoka na zawadi hiyo nono,Tamasha hilo liliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa. ameambatana na maafisa kutoka wizara hiyo pamoja na maafisa wa maendeleo ya michezo na utamaduni.
Asubuhi ya tamasha hilo ilipambwa na michezo ya asili kama vile kufukuza kuku, kukimbia na magunia, na kuvuka kamba, kabla ya mashabiki wa Simba na Yanga kucheza mchezo wa mpira wa miguu uliovuta hisia za wengi.
Baada ya michezo, burudani ya muziki ilichukua nafasi ambapo wasanii mbalimbali waliweka waliwasha moto jukwaani, akiwemo Isaya Michael maarufu kama Chino Kid, pamoja na mtumbuizaji bora wa Tuzo za Tanzania Music Awards (TMA) ambaye alipanda jukwaani na kuwaburudisha mashabiki.
Tamasha hilo lilifanyika kwa mafanikio makubwa likiwaleta pamoja wananchi wa rika tofauti kwa ajili ya kusherehekea utamaduni, michezo na burudani, sambamba na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza sekta ya sanaa na michezo nchini.