Maafisa Utamaduni Watakiwa Kuwasimamia Wasanii wa Mikoani ili Kukuza Sanaa

DAR ES SALAAM:MAAFISA Utamaduni nchini wametakiwa kuwajibika kikamilifu katika kuwasimamia wasanii waliopo katika mikoa mbalimbali ili kuhakikisha vipaji vyao vinatambulika na kustawi, badala ya kulazimika kuhamia Dar es Salaam kutafuta nafasi.
Wito huo umetolewa na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, alipokuwa akizungumza Leo April 24,2025 katika kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Maafisa Maendeleo ya Michezo kilichofanyika Tanzania.
Msigwa amesema kuwa kuna wasanii wengi wenye vipaji vikubwa mikoani, hususa ni katika tasnia ya vichekesho (comedy), lakini wanakosa msaada na ufuatiliaji kutoka kwa Maafisa Utamaduni wa maeneo yao.
“Mikoani kuna wasanii wengi sana hasa wa comedy ambao hawapati nafasi ya kujitangaza wala kupata mikopo. Hawa wanatakiwa wasimamiwe na Maafisa Utamaduni, lakini kwa bahati mbaya hamuwasimamii,” amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa ukosefu wa usimamizi wa karibu unasababisha wasanii hao wanapopata nafasi ya kuhamia Dar es Salaam wasiwe na hamu ya kurejea mikoani kwa kuwa hawakuwahi kupata sapoti kutoka kwa viongozi wa huko.
Aidha, Msigwa amesisitiza kuwa kila Afisa Habari anatakiwa kuwafahamu wasanii waliopo kwenye mkoa wake na kuhakikisha wanapata msaada wa kukuza kazi zao ili vipaji vyao visibaki bila kutambulika.