Ligi Kuu

TPLB imekanusha taarifa za Kariakoo Derby kuchezwa Mei 10 Zanzibar

DAR ES SALAAM: OFISA Habari wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Karim Boimanda, amekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kwamba mchezo wa Kariakoo Derby baina ya Simba na Yanga utachezwa Mei 10 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Boimanda amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote kwa sababu hadi sasa TPLB kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) hawajatangaza tarehe rasmi ya pambano hilo, ambalo liliahirishwa kutoka tarehe ya awali ya Machi 8 mwaka huu.

“Bado hatujatangaza tarehe rasmi ya mchezo huo, licha ya ukweli kwamba utachezwa kama sehemu ya ratiba ya ligi, tunawaomba wadau wa soka kupuuza taarifa hizo zisizo sahihi. Kama tulivyowatangazia awali, mchezo huo uliahirishwa na tarehe mpya tutaweka wazi pindi itakapopangwa rasmi,” amesema Boimanda.

Amesisitiza kuwa TPLB inaendelea kusimamia kwa makini ligi kwa kufuata miongozo na kanuni zilizowekwa na vyombo vya juu vya mpira wa miguu, ikiwemo TFF, CAF, na FIFA.

“Tunapokaribia ukingoni mwa msimu, presha huwa kubwa. Ndiyo maana tunazingatia kila hatua kuhakikisha ligi inamalizika kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea tangu mwanzo wa msimu,” amesema.

Boimanda ametoa wito kwa mashabiki wa soka kuwa watulivu na kusubiri taarifa rasmi kutoka mamlaka husika kuhusu ratiba ya mchezo huo mkubwa wa watani wa jadi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button