Majaliwa asema zawadi ya Rais Samia na Rais Mwinyi ni “Mitano Tena”

DAR ES SALAAM:WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema kuwa zawadi pekee ya thamani kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Hussein Mwinyi kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya michezo, sanaa na utamaduni ni kuwachagua tena kwa miaka mitano mingine, maarufu kama “mitano tena”.
Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Maendeleo ya Michezo wa Tanzania Bara, ambapo alisisitiza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya michezo chini ya uongozi wa viongozi hao wawili.
Amesema kuwa Tanzania imeshuhudia mafanikio makubwa, ikiwemo timu za taifa kama Taifa Stars, Serengeti Boys, na timu ya wanawake kufuzu kushiriki mashindano ya Afrika (AFCON).
Aidha, Waziri Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya AFCON 2027, alieleza kuridhishwa kwake na jitihada za Serikali katika maandalizi ya mashindano hayo ya kimataifa, ambayo Tanzania ni mwenyeji pamoja na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Amebainisha kuwa Serikali inajenga viwanja vipya na kufanya ukarabati mkubwa kwa viwanja vilivyopo ili kuhakikisha maandalizi ya miundombinu yanafikia viwango vya kimataifa.
Majaliwa amehitimisha kwa kusema kuwa maendeleo haya yanaonyesha dira njema ya nchi chini ya uongozi wa Rais Samia na Rais Mwinyi, hivyo kuwastahili kupewa fursa nyingine ya kuongoza kwa awamu nyingine.