Nyumbani

Fadlu asuka silaha za kuimaliza Stellenbosch, Sauz

DAR ES SALAAM:KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameweka wazi kuwa safu yake ya ushambuliaji inasukwa kwa umakini mkubwa kuelekea mchezo muhimu wa marudiano wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch FC utakaopigwa Jumapili, Aprili 27, katika Uwanja wa Moses Mabhida, Durban, Afrika Kusini.

Katika maandalizi hayo, nyota wa safu ya mbele ya Simba akiwemo Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua, Leonel Ateba na Kibu Denis, wamepewa majukumu maalumu kuhakikisha wanaiangusha Stellenbosch na kuipatia Tanzania nafasi ya pekee kwenye fainali ya CAF.

“Tunaenda kule kushambulia na kufunga, siyo kulinda bao moja. Dakika 10 za kwanza tutawapa presha kubwa wapinzani wetu,” amesema  Fadlu, akionesha wazi nia yake ya kusaka ushindi wa wazi ugenini.

Simba, ambao ndio wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki kwenye michuano hiyo, wanatarajia kuondoka nchini na msafara wa watu 60 kupitia ndege ya kukodi, wakiwa na malengo makubwa ya kuandika historia kwa kufuzu fainali.

Fadlu amesisitiza kuwa hawatacheza kwa kujilinda wala kutafuta sare, bali ushindi ndio ajenda kuu ya mchezo huo.

“Tayari tumeweka msingi nyumbani, sasa tunahitaji kwenda kumaliza kazi. Haitakuwa mechi rahisi, lakini tumejipanga kufanyia kazi mapungufu na kuhakikisha tunapata matokeo bora.” amesema

Mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla wanasubiri kwa hamu na tahadhari matokeo ya pambano hilo, ambalo linaweza kufungua ukurasa mpya katika historia ya soka la Tanzania.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button