Kamati ya TFF yapeleka kicheko Simba, kilio Yanga

DAR ES SALAAM, Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana kwa ajili ya kupitia na kutolea uamuzi mashauri mbalimbali ya ki soka yaliyowasilishwa mbele ya kamati hii imemuachia huru Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally na kumtoza faini ya shilingi milioni 5 Msemaji wa Klabu ya Yanga Ally Kamwe.
Ahmed Ally ambaye aliitwa katika kamati hiyo baada ya kushtakiwa na klabu ya Yanga akituhumiwa kwa kosa la kuchochea umma kwa ujumla kinyume na Kanuni 73(4) ya Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la Mwaka 2021.
Taarifa iliyotolewa na TFF imeeleza kuwa, Baada ya kupitia maelezo ya pande zote husika pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa mbele yake, Kamati ilibaini kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kwa kosa aliloshtakiwa nalo na hivyo imemuachia huru.
Kwa upande wa Ally Kamwe, aliyeshtakiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi akituhumiwa kwa kosa la kuchochea umma kwa ujumla kinyume na Kanuni 73(4) ya Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la Mwaka 2021.
Kamati hiyo imesema kuwa, Baada ya kusikiliza pande zote na kupitia nyaraka na vielelezo vilivyowasilishwa mbele yake, imemtia hatiani kwa kosa aliloshtakiwa nalo na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi milioni 5 na onyo la kutofanya kosa la kimaadili ndani ya kipindi cha miaka miwili. Adhabu hiyo tayari imeanza tarehe 16/04/2025.